RAIS RUTO AFUNGUA RASMI MAONYESHO YA KILIMO MOMBASA
By Dayo Radio
Published on 04/09/2025 14:21
News

Rais William Ruto amefungua rasmi Maonyesho ya Kilimo ya Mombasa (ASK International Show) katika uwanja wa maonyesho wa Mkomani, Kaunti ya Mombasa.

Maonyesho hayo yaliyoanza Septemba 3 na kutarajiwa kukamilika Septemba 7, 2025, yanafanyika chini ya kauli mbiu “Promoting Climate-Smart Agriculture and Trade Initiative for Sustainable Economic Growth”. Lengo kuu ni kuhamasisha mbinu za kilimo endelevu na kuimarisha ukuaji wa kiuchumi.

Shughuli hiyo imevutia zaidi ya washiriki 1,000 wakiwemo wakulima, mashirika ya kiserikali, kampuni binafsi pamoja na wadau wa kimataifa. Washiriki wameonyesha ubunifu na teknolojia za kisasa katika sekta ya kilimo, mifugo na biashara.

Akihutubia wageni na wananchi waliohudhuria, Rais Ruto alisisitiza kuwa serikali yake imejitolea kuwekeza katika teknolojia na mbinu bunifu za kilimo ili kuwasaidia wakulima kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza uzalishaji.

Maonyesho ya Mombasa yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwaleta pamoja wakulima, wawekezaji na wananchi kwa lengo la kukuza sekta ya kilimo na kuchochea maendeleo ya taifa.

Comments
Comment sent successfully!