Na Rajab Waziri
MOMBASA, Julai 11, 2026
Vijana katika eneo bunge la Nyali, Kaunti ya Mombasa, wamehimizwa kujiepusha na matumizi ya mihadarati na kukumbatia amani ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali za maendeleo zinazotolewa na serikali ya kaunti pamoja na serikali ya kitaifa.
Wito huo ulitolewa wakati wa hafla ya kukabidhi vyeti kwa vijana wa kundi la Mnazi Mmoja Youth Reformers, ambao wamefanikiwa kujinasua kutoka katika matumizi ya dawa za kulevya kupitia programu za marekebisho na uwezeshaji.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kiongozi wa Vijana wa Nyali, Elkana Jacob, alisema matumizi ya mihadarati yamekuwa chanzo cha umaskini, ukosefu wa ajira na kuharibu mustakabali wa vijana wengi. Aliwataka wale wanaokabiliwa na changamoto hiyo kutafuta99 msaada na kuanza upya maisha yenye tija.

Jacob pia aliwahimiza vijana kutoruhusu kutumiwa na wanasiasa kuchochea vurugu, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii.
"Hatutaki vijana wetu watumiwe kueneza vurugu na taharuki. Wale wanaowatumia vijana kwa uhalifu wajue sheria itachukua mkondo wake," alisema Jacob.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mombasa Youth Council, Jonhs Suka, aliitaka jamii kuwakaribisha na kuwaunga mkono vijana walioamua kuachana na matumizi ya mihadarati na uhuni badala ya kuwabagua.
"Jamii iwapokee kwa mikono miwili vijana hawa ili wapate nafasi ya kujijenga upya na kuwa sehemu ya maendeleo ya jamii," alisema Suka.
Naye Abubakar Abuu alisema juhudi za kuwaunganisha vijana kutoka maeneo mbalimbali zimechangia kupunguza migogoro iliyokuwepo hapo awali.
"Leo vijana wa Kisumu Ndogo na Mnazi Mmoja tunaishi kwa umoja. Zamani tulikutana kwa mapanga, lakini sasa tumeamua kujenga amani na kushirikiana," alisema.
Mkurugenzi wa Shirika la Amkeni, Christine Khabuya, alisema shirika hilo litaendelea kushirikiana na vijana hao kwa kuwapatia ushauri nasaha, huduma za kisaikolojia pamoja na mafunzo ya kuwawezesha kurejea katika maisha ya kawaida na kujitegemea.
Katika hafla hiyo, vijana waliokamilisha programu hiyo walikabidhiwa mkokoteni pamoja na vifaa vya ukusanyaji taka kupitia Elkana Jacob Foundation ili kuwawezesha kuanzisha shughuli za kujipatia kipato na kujitegemea kiuchumi.
Waandalizi wa programu hiyo walisema juhudi za kuwawezesha vijana kiuchumi na kuwapa matumaini mapya ni hatua muhimu katika kupambana na matumizi ya mihadarati, kuimarisha usalama na kujenga jamii yenye amani na maendeleo endelevu.